Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imerejea rasmi katika mauzo ya nje ya kobalti baada ya kuyasitisha kwa kipindi cha miezi 10, hatua iliyolenga kudhibiti kushuka kwa bei ya madini hayo kufuatia kuongezeka kwa usambazaji katika soko la dunia.
Serikali ya DRC ilitangaza Jumanne kuwa uamuzi wa kurejesha mauzo ya kobalti umeanza kutekelezwa, baada ya kusitishwa huko awali kulikokusudia kuleta utulivu wa bei katika soko la kimataifa.
DRC ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa kobalti, madini muhimu yanayotumika katika utengenezaji wa betri za kisasa, ikiwemo betri za simu za mkononi na magari ya umeme.
Awali, marufuku ya kuuza nje kobalti ilianzishwa kwa miezi minne kabla ya kuongezwa muda, ikiwa na lengo la kukabiliana na wingi wa usambazaji uliokuwa ukisababisha kuporomoka kwa bei.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Fedha wa DRC, Doudou Fwamba, alisema kuwa kuanzia Ijumaa iliyopita, nchi hiyo imeanza tena kusafirisha kobalti yake nje ya nchi.
Alifafanua kuwa hatua ya kusitisha mauzo ililenga kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha udhibiti wa kitaifa juu ya rasilimali zake za madini.
Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, DRC ilichangia takribani asilimia 76 ya uzalishaji wa kobalti duniani mwaka 2024.
Fwamba alieleza kuwa haikuwa sahihi kwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa madini hayo kukosa ushawishi katika upangaji wa bei za soko la kimataifa.
Serikali ilisema kushuka kwa bei kulichangiwa zaidi na ongezeko la uzalishaji kutoka kwa kampuni ya madini ya China, CMOC, inayomiliki na kuendesha migodi mikubwa ya Tenke Fungurume na Kisanfu nchini DRC.
Waziri huyo aliongeza kuwa DRC ilipoteza mapato makubwa kutokana na kushuka kwa bei ya kobalti, lakini akabainisha kuwa mkakati wa kusitisha mauzo, ulioratibiwa na shirika la serikali la ARECOMS, umezaa matunda.
Kwa mujibu wa serikali, bei ya kobalti imeongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka takribani dola 22,000 kwa tani hadi kati ya dola 54,000 na 55,000 kwa tani.
Kobalti nyingi nchini DRC hupatikana katika migodi ya mkoa wa Katanga kusini-mashariki mwa nchi, eneo ambalo kwa kiasi kikubwa limeepuka athari za migogoro ya silaha inayokumba mikoa ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako waasi wa M23 wanadhibiti maeneo kadhaa.
CHANZO: TRT afrika














