Umoja wa Ulaya umeeleza kuwa uhuru, umoja wa kitaifa na uadilifu wa mipaka ya Somalia vinapaswa kulindwa, kufuatia tangazo la Israel la kulitambua eneo la Somaliland kama taifa huru.
Israel ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa imechukua uamuzi wa kuitambua rasmi Somaliland, hatua iliyozua mjadala na upinzani kutoka mataifa na mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, msemaji wa masuala ya nje Anouar El Anouni alisema muungano huo unaendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa mamlaka ya Somalia kwa mujibu wa Katiba yake pamoja na misingi ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Aliongeza kuwa kulinda umoja wa Somalia ni jambo muhimu kwa kudumisha amani na utulivu katika eneo la Pembe ya Afrika.
Aidha, Umoja wa Ulaya ulihimiza kufanyika kwa mazungumzo ya dhati kati ya Somaliland na Serikali ya Shirikisho ya Somalia, kwa lengo la kutatua tofauti zilizodumu kwa muda mrefu kwa njia ya amani.
Hatua ya Israel ilipingwa vikali na serikali ya Somalia, ambayo iliitaja kama kitendo cha makusudi kinachokiuka mamlaka yake. Nchi kadhaa zikiwemo Misri, Uturuki, Baraza la Ushirikiano la Ghuba pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu pia zililaani uamuzi huo.
CHANZO: TRT Afrika














