Mahakama ya shirikisho nchini Marekani imesitisha kwa muda utekelezaji wa mpango wa serikali ya Rais Donald Trump wa kuwafukuza wahamiaji kutoka Sudan Kusini, ikisubiri uamuzi wa mwisho wa kesi inayopinga hatua hiyo.
Jaji wa Wilaya ya Marekani, Angel Kelley, alitoa amri ya muda siku ya Jumanne akizuia kufutwa kwa hadhi ya ulinzi wa muda (TPS) kwa raia wa Sudan Kusini, hatua ambayo ingeruhusu kuanza kwa kufukuzwa kwa wahamiaji hao kuanzia tarehe 6 Januari 2026. Uamuzi huo unamaanisha kuwa raia hao wataendelea kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kisheria hadi kesi hiyo itakaposikilizwa kikamilifu.
Takribani raia 300 wa Sudan Kusini waliokuwa chini ya mpango wa TPS, au waliokuwa na maombi yanayoendelea, wangepoteza haki zao za kisheria na kukabiliwa na hatari ya kurejeshwa nchini mwao endapo mpango huo ungetekelezwa.
Mashirika ya kutetea haki za kiraia yaliwasilisha kesi dhidi ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (DHS), yakidai kuwa uamuzi wa kufuta TPS ulikiuka taratibu za kisheria za utawala na Katiba ya Marekani, na ulilenga kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupunguza idadi ya wahamiaji wasio wazungu na wasio wa Ulaya nchini humo.
Katika uamuzi wake, Jaji Kelley alisema hatua hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa na yasiyoweza kurekebishwa kwa wahamiaji wa Afrika Mashariki, hivyo ikahitaji uchambuzi wa kina wa kisheria kabla ya kutekelezwa.
Hata hivyo, Wizara ya Usalama wa Ndani ilipinga vikali uamuzi huo, ikisema mahakama inaingilia mamlaka ya kikatiba ya rais. DHS ilidai kuwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini imeimarika na kwamba kuna mipango ya kuhakikisha raia wanaorejea wanaunganishwa salama na jamii zao.
Hadhi ya ulinzi wa muda kwa raia wa Sudan Kusini ilianza kutumika mwaka 2011 kufuatia migogoro ya muda mrefu, hali ambayo imeifanya nchi hiyo kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya kibinadamu.
Hatua hii ni sehemu ya sera pana za utawala wa Trump zinazolenga kupunguza ulinzi wa kisheria kwa wahamiaji, ikiwa ni pamoja na juhudi za kufuta TPS kwa raia wa nchi kadhaa kama vile Venezuela, Haiti, Afghanistan, Syria na Honduras.
CHANZO: TRT Afrika














