Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, amesema Cairo haitasita kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kulinda umoja na uadilifu wa Sudan, ambayo sasa inakaribia kuingia mwaka wa nne wa mapigano kati ya jeshi na vikosi vya RSF.
Akizungumza mjini Cairo pamoja na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan, Ramtane Lamamra, Abdelatty alisisitiza kuwa kuanguka kwa taasisi za Sudan au kuvunjika kwa umoja wa taifa hilo ni “mstari mwekundu” kwa Misri.
Kauli hiyo inalingana na msimamo wa Rais Abdel Fattah al-Sisi, ambaye mwezi uliopita alionya kuwa tishio lolote kwa taasisi za Sudan ni sawa na tishio kwa usalama wa Misri. Taarifa kutoka ofisi yake iliongeza kuwa Misri imehifadhi haki ya kuchukua hatua zote zinazohitajika chini ya sheria za kimataifa, ikiwemo uwezekano wa makubaliano ya ulinzi wa pamoja.
Misri na Sudan zina historia ndefu ya ushirikiano wa kijeshi, ikiwemo mkataba wa ulinzi wa mwaka 1976 na makubaliano ya mafunzo na usalama wa mipaka yaliyosainiwa Machi 2021.
CHANZO: TRT Afrika














