Kundi la waasi wa Alliance Fleuve Congo/M23 limetangaza kuwa limeweka mji wa Uvira, jimbo la Sud-Kivu, chini ya “uwajibikaji wa kimataifa” baada ya kuondoa vikosi vyake mnamo Desemba 15, 2025. Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kundi hilo limesisitiza kuwa halitahusika tena na usalama wa mji huo na linaitaka MONUSCO kutekeleza jukumu lake la kulinda raia.
Corneille Nangaa, mratibu wa kisiasa wa AFC/M23, ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa utata kuhusu dhamira ya kundi hilo kuunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano na kutafuta suluhu ya kisiasa. Hata hivyo, ametoa tahadhari kuhusu uwepo wa vikundi vya silaha vinavyotajwa kuwa tishio, ikiwemo jeshi la Burundi, waasi wa FDLR, makundi ya Wazalendo na “wajeda wa kulipwa” wanaosaidia jeshi la serikali.
AFC/M23 imetaka Umoja wa Mataifa kupeleka “nguvu ya upande wa tatu” ili kuzuia Uvira kurudi katika machafuko, ikisisitiza kuwa lengo ni kulinda raia na kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hatua hii inakuja wakati juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Marekani bado hazijazaa matunda, licha ya makubaliano yaliyotiwa saini na Rais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda. Mazungumzo ya Doha chini ya usimamizi wa Qatar yamekwama, huku hatua zilizokubaliwa zikiwa hazijatekelezwa.
Wakati mapigano yakiendelea, Angola imeanza tena kujihusisha na mchakato wa amani, na Togo inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa juu wa viongozi Januari 17, 2026. Rais wa Angola João Lourenço, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, amekutana na viongozi wa dini wa Congo na kusisitiza haja ya mazungumzo ya kitaifa jumuishi kwa ajili ya amani ya kudumu.
CHANZO: AA














