Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria, akieleza matumaini kuwa hatua hiyo itafungua njia ya suluhu ya kudumu bila umwagaji damu zaidi. Akihutubia bungeni, Erdogan alisema Uturuki imekuwa ikisisitiza kuhifadhi Syria kama taifa lenye mamlaka kamili na mshikamano wa kisiasa.
Makubaliano hayo yalitangazwa na serikali ya Syria pamoja na kundi la YPG, yakitoa muda wa siku nne wa kutekeleza mpango wa ushirikiano katika eneo la Hasakah. Erdogan alionya kuwa jaribio lolote la kuvuruga utulivu litakuwa sawa na kujitoa muhanga, akisisitiza kuwa uthabiti lazima udumishwe.
Aidha, alibainisha kuwa utulivu wa Syria utawanufaisha zaidi Wakurdi wa Syria na kuongeza kuwa Uturuki haina nia ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, lakini haitakubali maslahi yake kudhoofishwa. Erdogan pia alisema amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu juhudi za pamoja za kupambana na Daesh na kuimarisha usalama wa Syria.
CHANZO: TRT Afrika














