Mfalme Mohammed VI wa Morocco amesisitiza kuwa mshikamano wa mataifa ya Afrika utaendelea licha ya mvutano uliotokea katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kati ya Morocco na Senegal. Alieleza kuwa undugu wa kihistoria na ushirikiano wa manufaa uliojengwa kwa muda mrefu hauwezi kutetereka kwa sababu ya tukio moja la michezo.
Fainali hiyo ilikumbwa na sintofahamu baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani wakipinga penati iliyotolewa kwa Morocco dakika za mwisho, kabla ya kurejea na kushinda 1–0 katika muda wa ziada. Tukio hilo lilisababisha vurugu kati ya mashabiki na kuibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii.
Senegal imekuwa mshirika wa karibu wa Morocco kwa muda mrefu, hasa kupitia uwekezaji wa kampuni na benki za Morocco, jambo lililoimarisha ushawishi wa kidiplomasia wa Rabat barani Afrika. Mfalme Mohammed VI pia alitaja mashindano hayo kama mafanikio kwa bara zima, akionyesha maendeleo ya Morocco na mchango wake kwa michezo ya Afrika.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesema litachukua hatua baada ya kuchunguza matukio ya mechi hiyo, huku Rais wa FIFA Gianni Infantino akilaani tabia ya baadhi ya wachezaji wa Senegal na benchi lao la ufundi.
CHANZO: TRT Afrika














