Ghana imeamua kuanza kusafisha dhahabu ndani ya nchi badala ya kuendelea kuuza malighafi, hatua inayolenga kuongeza mapato, ajira na fedha za kigeni. Hii inafuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya Gold Board (GoldBod) na kampuni ya Gold Coast Refinery Limited, ambayo yatawezesha usafishaji wa kilo 52,000 za dhahabu kwa mwaka kabla ya kusafirishwa nje.
Mpango huo utaanza rasmi Februari 1, 2026, na awamu ya kwanza itahusisha dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati. Serikali ya Ghana itapata asilimia 15 ya faida bila malipo kutoka kwa uwekezaji wa Gold Coast Refinery. Kila bati ya dhahabu itabeba alama za GoldBod, Mamlaka ya Viwango Ghana, Benki Kuu ya Ghana na Gold Coast Refinery, kulingana na viwango vya kimataifa.
Ushirikiano huu pia unahusisha Rand Refinery, kiwanda pekee barani Afrika kilichoidhinishwa na London Bullion Market Association (LBMA), ambacho kitatoa msaada wa kiufundi na kibiashara huku Ghana ikijipanga kupata ithibati yake ya LBMA. Hatua hii itaiwezesha nchi kusafisha dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wakubwa kwa ajili ya masoko ya kimataifa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa GoldBod, Sammy Adu Gyamfi, alisema kuwa karibu asilimia 99.9 ya dhahabu ya Ghana imekuwa ikisafirishwa ghafi, jambo ambalo sasa linabadilika. Aliongeza kuwa usafishaji wa ndani utaongeza mapato ya kodi, kuimarisha ufuatiliaji wa dhahabu na kuunda nafasi nyingi za ajira. Pia alisisitiza kuwa mamilioni ya dola yaliyokuwa yakilipwa kwa viwanda vya usafishaji nje ya nchi sasa yatabaki ndani ya uchumi wa Ghana.
CHANZO: TRT Afrika














