Serikali ya Uganda imetangaza Januari 15 na 16, 2026 kuwa siku za mapumziko ili wananchi zaidi ya milioni 21.6 washiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu. Wapiga kura watachagua viongozi kuanzia ngazi ya urais, wabunge hadi serikali za mitaa.
Kuna wagombea 8 wa urais, akiwemo Rais Yoweri Museveni anayewania awamu ya saba. Idadi ya wapiga kura imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo waliosajiliwa walikuwa milioni 18.1.
Hata hivyo, uchaguzi utafanyika bila huduma ya intaneti baada ya Tume ya Mawasiliano ya Uganda kusimamisha mtandao na uuzaji wa kadi mpya za simu kuanzia Januari 13, hatua iliyolenga kupunguza taarifa potofu mtandaoni. Hatua hiyo imekosolewa na mashirika ya haki za binadamu na vyama vya upinzani wakisema inaweza kuathiri uwazi wa uchaguzi.

Serikali pia imeamuru mashirika mawili ya haki za kiraia kusitisha shughuli zao: Chapter Four Uganda na Human Rights Network for Journalists. Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, COMESA, IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari wako nchini kufuatilia mchakato wa kura.
Tume ya Uchaguzi imewaonya wapiga kura kutovaa mavazi yenye rangi au ujumbe wa vyama vya kisiasa. Aidha, mfumo wa uthibitishaji wa wapiga kura kwa mashine za kielektroniki utatumika, zikiwa na uwezo wa kufanya kazi kwa saa 20 mfululizo ili kuhakikisha zoezi linaenda vizuri.
CHANZO: TRT Afrika














