Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa shilingi milioni 100 za Kitanzania ili kukamilisha ujenzi wa makumbusho ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli.
Taarifa hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais, Emmanuel Nchimbi, wakati wa ibada ya kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha kiongozi huyo iliyofanyika tarehe 17 Machi 2026.
Alisema kuwa Rais Samia amekuwa akifuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa makumbusho hayo yaliyopo Chato, na baada ya kubaini kuwa fedha zilizobaki kukamilisha mradi huo ni milioni 100, aliamua kuzitoa zote.
Makumbusho hayo yanatarajiwa kuwa kituo muhimu cha kuhifadhi historia ya maisha, uongozi na mafanikio ya Hayati Magufuli, yakitoa fursa kwa vizazi vya sasa na vijavyo kujifunza mchango wake katika maendeleo ya taifa.
John Pombe Magufuli, maarufu kama JPM, alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021 katika hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam, kutokana na maradhi ya moyo.
CHANZO: TRT Afrika














