Uturuki Ajenda

Uturuki Yaanzisha Kanuni Mpya za Kulinda Watoto Katika Mitandao ya Kijamii

Sheria mpya zaweka masharti makali kwa makampuni ya mitandao kuhakikisha usalama wa vijana.

Newstimehub

Newstimehub

23 Aprili, 2026

660

Uturuki imeanza kutekeleza kanuni mpya za mitandao ya kijamii zenye lengo la kuongeza ulinzi kwa watoto na vijana wanapotumia majukwaa ya mtandaoni.

Kanuni hizo zimekuja kama sehemu ya juhudi za kuongeza usalama wa watumiaji, uwajibikaji wa kampuni za mitandao na uondoaji wa haraka wa maudhui yenye madhara. Hatua hiyo inaifanya Uturuki kujiunga na nchi nyingine kama Australia na Ufaransa ambazo tayari zimechukua hatua zinazofanana.

Kwa mujibu wa sheria mpya, watoto walio chini ya miaka 15 hawataruhusiwa kujisajili katika mitandao ya kijamii. Kampuni za mitandao zitahitajika kuweka mfumo wa uhakika wa kuthibitisha umri wa watumiaji wao.

Aidha, watoa huduma watalazimika kutoa huduma tofauti kwa watumiaji walio chini ya miaka 15 na wale walio juu ya umri huo, ili kuhakikisha ulinzi unaofaa kwa kila kundi.

Serikali pia imeweka mfumo wa utekelezaji wa hatua kwa hatua. Kwanza, kampuni zitahitajika kufuata masharti ya msingi; iwapo zitakiuka, matangazo mapya katika mitandao hiyo yanaweza kupigwa marufuku. Ukiukaji ukiutokea tena, mamlaka zinaweza kuomba idhini ya mahakama kupunguza kasi ya huduma hadi asilimia 50, na baadaye hadi asilimia 90.

Sheria hizo pia zinahusisha mitandao ya michezo, hasa ile ambayo haina udhibiti wa umri, huku tovuti za michezo za kigeni zenye watumiaji wengi zikitakiwa kuwa na mwakilishi wa kisheria nchini Uturuki.

Kanuni hizi mpya zitaanza kufanya kazi miezi sita baada ya kutangazwa.

CHANZO: TRT Afrika