Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa mapato ya mauzo ya madini na mali za serikali, akionya kuwa udhibiti dhaifu unaikosesha nchi kunufaika ipasavyo na ongezeko kubwa la mauzo ya madini.
Kwa mujibu wa taarifa ya baraza la mawaziri, Tshisekedi alisema kuwa licha ya nchi hiyo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa duniani wa cobalt na shaba, bado serikali inapoteza mapato kutokana na usimamizi hafifu, ubia usio wazi katika migodi ya serikali, na uhamishaji haramu wa mitaji nje ya nchi.
Mwaka 2025, DRC ilisafirisha tani milioni 3.4 za shaba na tani 220,000 za cobalt, kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.
Rais huyo ameagiza ukaguzi huo kukamilika ndani ya siku 30 ili kubaini mapato ambayo hayajalipwa na mapungufu ya kiutawala katika sekta ya madini.
CHANZO: TRT Afrika














