Wanawake wawili kutoka Sudan wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafıria kuzidiwa na idadi ya watu wakati wakijaribu kuvuka bahari kutoka kaskazini mwa Ufaransa kuelekea Uengereza.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za uokoaji, boti hiyo ndogo ilikuwa imebeba wahamiaji wengi kuliko uwezo wake, hali iliyosababisha matatizo makubwa katikati ya safari. Wanawake hao walipoteza maisha kutokana na hali mbaya ya safari hiyo, ikiwemo msongamano, ukosefu wa hewa ya kutosha na uchovu uliokithiri.
Mashirika ya uokoaji yameeleza kuwa juhudi zilifanyika kuwaokoa abiria wengine waliokuwa ndani ya boti hiyo, na wengi wao walinusurika lakini wakiwa katika hali mbaya kiafya. Tukio hilo limeongeza idadi ya vifo vinavyotokana na safari hatari za wahamiaji wanaojaribu kuvuka bahari kuelekea Ulaya Magharibi.
Wahamiaji wengi wanaochukua njia hiyo hutoka katika maeneo yenye migogoro na umaskini, wakitafuta maisha bora, lakini hukutana na hatari kubwa ikiwemo ajali za majini, hali mbaya ya hewa na ukosefu wa msaada wa haraka.
Serikali na mashirika ya kimataifa yameendelea kutoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti ili kuzuia vifo vya aina hii, ikiwa ni pamoja na kuboresha njia salama za uhamiaji na kushughulikia sababu zinazowasukuma watu kuhama.
Chanzo:Africanews

















