Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa toleo la makubaliano yaliyopendekezwa kati ya Marekani na Iran kuhusu kusitisha vita, sio kama lilivyoelezwa na Iran.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social Ijumaa, Trump alisema kuwa ripoti za vyombo vya habari kuhusu masharti ya waraka wa maelewano kati ya Marekani na Iran zilikuwa si sahihi.
“Masharti ambayo Iran ilivujisha kwa vyombo vya habari potofu (Fake News) hayana uhusiano wowote na masharti yaliyokubaliwa kwa maandishi,” aliandika.
“Walichosema, pamoja na taarifa yao dhaifu na ya kusikitisha kwamba makubaliano yamefikiwa, hakina uhusiano wowote na ukweli. Ni watu wasio waaminifu sana kufanya nao mazungumzo. Kwao, hakuna kitu kama kufanya mazungumzo kwa nia njema. INASHANGAZA! Pia, shambulio lao la ndege zisizo na rubani jana usiku dhidi ya meli za India zilizokuwa zikiondoka katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ambalo lilizuiwa, halikubaliki kabisa. Wanapaswa kujirekebisha, na haraka!”
Pande zote zinatofautiana
Shirika rasmi la habari la Iran, Islamic Republic News Agency, hapo awali lilichapisha kile lilichokiita rasimu ya waraka wa maelewano wenye vipengele saba, ambayo ilitofautiana na toleo la makubaliano lililoripotiwa awali na vyombo vya habari vya Marekani.
IRNA ilisema kuwa Iran haitachukua masharti mapya kuhusu nyuklia na itaendelea kuwa na mamlaka kamili juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz. Hata hivyo, Shirika la Habari la Axios liliripoti kuwa mfumo wa makubaliano ulijumuisha suala la akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran pamoja na “kufunguliwa mara moja” kwa njia hiyo ya maji bila ya kutoza ushuru.
Kwa mujibu wa ripoti ya Iran, nchi hiyo haitatoa ahadi yoyote ya kuhamisha udhibiti wa Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa majini ambayo Iran imekuwa ikiidhibiti kwa karibu tangu hatua za mwanzo za mzozo huo.
Badala yake, suala hilo lingeshughulikiwa kupitia mazungumzo na maamuzi ya pamoja kati ya Iran na Oman.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema Alhamisi kwamba sehemu kuu ya waraka ya makubaliano ilikuwa imekamilishwa, huku ikiishutumu Mareknai kwa kudhoofisha maendeleo ya mazungumzo kupitia misimamo inayokinzana.

















