Michezo

Tunisia yamteua kocha Herve Renard baada ya kipigo cha Sweden

Shirikisho la Soka la Tunisia (FTF) limesema kuwa Hervé Renard atakuwa kocha wa timu hiyo hadi mwisho wa kampeni yao ya Kombe la Dunia.

Newstimehub

Newstimehub

16 Juni, 2026

1781604941484 fjxy0cb 598b1c329cafa427f869ce4fca84cd37b0174297aab0fa7dd53bbe43972fe65e

Tunisia imemfuta kazi kocha Sabri Lamouchi na kumteua Hervé Renard kuchkua nafasi yake, Shirikisho la Soka la Tunisia (FTF) limetangaza.

Haya yanajiri baada ya Tunisia kupata kipigo cha mabao 5-1 katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia dhidi ya Sweden iliyochezwa Jumapili.

Lamouchi, ambaye ndiye kocha wa kwanza kufutwa kazi katika mashindano hayo, aliteuliwa Januari kwa mkataba wa kuinoa timu hiyo hadi mwaka 2028. Tunisia sasa itamenyana na Japan siku ya Jumamosi na Uholanzi tarehe 25 Juni.

Chini ya Lamouchi, Tunisia ilishinda mechi moja tu kati ya tano, ikiifunga Haiti 1-0 mwezi Machi. Pia ilipoteza 1-0 dhidi ya Austria na kuchapwa 5-0 na Ubelgiji katika mechi mbili za kirafiki za maandalizi ya Kombe la Dunia mwezi huu.

 Katika taarifa iliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii Jumanne, FTF ilisema kuwa Renard ataiongoza Tunisia hadi mwisho wa kampeni yao ya Kombe la Dunia.

“Makubaliano hayo pia yanaeleza kuwa mazungumzo yataanzishwa baada ya kampeni ya Kombe la Dunia ili kuangalia uwezekano wa ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia malengo maalum ya kimichezo,” iliongeza taarifa hiyo.

Shirika la utangazaji la serikali ya Tunisia, Television Tunisienne, liliripoti kuwa Renard atawasili Monterrey baadaye Jumanne ili kujiunga na kikosi hicho.

Renard, ambaye amewahi kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara mbili, 2012 na 2015, pia aliifundisha Saudi Arabia katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar na kuiongoza kupata ushindi maarufu dhidi ya Argentina, ambao baadaye walikuja kuwa mabingwa wa dunia, katika hatua ya makundi.

Baadaye aliondoka kwenda kuifundisha timu ya wanawake ya Ufaransa katika Kombe la Dunia la Wanawake la 2023 na Michezo ya Olimpiki ya Paris, kabla ya kurejea Saudi Arabia na kusaidia timu ya wanaume kufuzu kushiriki katika Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo.

Baadaye nafasi yake ilichukuliwa na Georgios Donis.