Jeshi la Marekani limesema limeanzisha mashambulizi dhidi ya Iran kujibu “majaribio ya Iran kushambulia” wanajeshi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM).
Jeshi hilo limeongeza kuwa limeshambulia vituo kadhaa vya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) mapema Alhamisi, baada ya kile lilichokitaja kuwa majaribio ya Iran kurusha makombora dhidi ya majeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Katika taarifa yake, CENTCOM imesema vikosi vyake vimeshambulia vituo vya uongozi wa kijeshi, maeneo ya makombora na ndege zisizo na rubani, vituo vya ufuatiliaji na ulinzi wa pwani, pamoja na miundombinu ya kijeshi ya majini katika maeneo mbalimbali nchini Iran.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa operesheni hiyo, imelenga kupunguza vitisho vinavyotokana na Iran na makundi yanayoiunga mkono dhidi ya majeshi ya Marekani, usafiri wa meli za kibiashara na mataifa jirani ya Ghuba.
Kwa mujibu wa jeshi la Marekani, mashambulizi hayo yalifuatia hatua ya IRGC kurusha makombora kadhaa ya balestiki kutoka Iran tarehe 28 Julai katika kile ilichokitaja kuwa jaribio la kushtukiza kushambulia majeshi ya Marekani yaliyoko katika eneo hilo.
CENTCOM imesema zaidi ya wanajeshi 50,000 wa Marekani bado wamepelekwa Mashariki ya Kati na wako katika hali ya tahadhari ya juu huku mvutano ukiendelea kuongezeka kufuatia mashambulizi ya pande zote yaliyotokea hivi karibuni.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti milipuko kadhaa kusini mwa nchi hiyo, huku milipuko ikisikika katika mji wa bandari wa Bandar Abbas na mashambulizi mengine yakiripotiwa kwenye Kisiwa cha Qeshm.
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeongezeka katika wiki za hivi karibuni, ambapo Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya Iran, huku Iran nayo ikijibu kwa kulenga vituo na vifaa vya kijeshi vya Marekani vilivyopo katika nchi mbalimbali za eneo hilo.
“Tutawashambulia kwa nguvu”
Mashambulizi ya hivi karibuni yamefanyika saa chache baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia meli ya kubeba gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) inayomilikiwa na Marekani nchini Misri.
Mapema siku hiyo, Rais Donald Trump amesema jeshi la Marekani litaishambulia Iran “kwa nguvu” baada ya shambulio la kombora dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Jordan, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fox News.
“Tutawashambulia kwa nguvu. Watapata kipigo kikubwa,” mwandishi wa Fox News alimnukuu Trump akisema Jumatano, akiongeza kuwa rais huyo alitumia lugha chafu kusisitiza msimamo wake akisema: “Tutawapiga vibaya sana.”
Trump pia ameliambia shirika hilo la habari kwamba mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Saudi Arabia dhidi ya wanamgambo wanaoiunga mkono Iran nchini Iraq usiku uliopita yaliratibiwa na mamlaka za Iraq, licha ya serikali ya Iraq kulaani mashambulizi hayo hadharani.
“Mashambulizi hayo yaliratibiwa na serikali ya Iraq,” mwandishi wa Fox News alisema baada ya kuzungumza na kiongozi huyo wa Marekani.

















