Kesi ya mauaji ya mwanamuziki mashuhuri wa rap, Tupac Shakur, haikutatuliwa kwa miongo kadhaa. Sasa, mtu anayeshtakiwa kwa kuhusika na mauaji yake yaliyotokea Las Vegas mwaka 1996 kesi yake imeanzwa kusikilizwa mahakamani.
Duane “Keffe D” Davis, mwenye umri wa miaka 63, anakabiliwa na shtaka moja la mauaji kwa kutumia silaha hatari, huku akidaiwa kuwa na nia ya kuchangia, kuendeleza au kusaidia shughuli za genge la uhalifu katika kifo cha Shakur. Uchaguzi wa majaji utaanza Jumatatu, huku kesi hiyo ikitarajiwa kuchukua takribani mwezi mmoja.
Kesi hiyo inatarajiwa kufichua zaidi moja ya mafumbo makubwa katika ulimwengu wa muziki wa hip-hop ambayo yamewavutia watu kwa miongo kadhaa. Shakur, ambaye pia alitumia majina ya kisanii 2Pac na Makaveli, anachukuliwa kuwa mmoja wa wasanii wa rap wenye ushawishi mkubwa.
Shakur alipigwa risasi mjini Las Vegas Septemba 7, 1996. Wakati huo alikuwa kwenye gari jeusi aina ya BMW pamoja na gwiji wa muziki Marion “Suge” Knight, wakielekea Club 662 ambako Shakur alikuwa amepangiwa kutumbuiza. Gari jeupe aina ya Cadillac liliwasogelea pembeni, kisha risasi zikaanza kurushwa.
Tupac Shakur, aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha abiria, alipigwa risasi mara kadhaa na kufariki dunia siku sita baadaye. Knight alinusurika katika tukio hilo.
Historia ya maisha yake
Kesi hiyo ilikwama kwa miaka mingi hadi katika miaka ya hivi karibuni, wakati taarifa za hadharani pamoja na kitabu cha historia cha Davis kilichofichua mambo mengi kuhusu maisha yake vilipoibua upya suala hilo.
Wakati wa kifo cha Tupac Shakur, Davis alikuwa kiongozi wa genge la South Side Compton Crips. Alikamatwa mwaka 2023 na kukana mashtaka dhidi yake.
Mambo muhimu kuhusu kesi hiyo
Uchaguzi wa majaji utaanza Jumatatu na unatarajiwa kuchukua siku kadhaa. Baada ya hapo, upande wa mashtaka na upande wa utetezi utatoa hoja zao za mwanzo, kabla ya ushahidi kuanza kutolewa.
Ndani ya mahakama, nafasi za wananchi wanaotaka kufuatilia kesi hiyo zitakuwa chache. Kutakuwa na bahati nasibu kila siku kwa ajili ya kuwapa baadhi ya watu nafasi ya kuingia mahakamani. Chumba kilichopo ghorofa ya pili ya mahakama pia kitafunguliwa kwa umma na kitaonyesha matangazo ya moja kwa moja ya mwenendo wa kesi.
Huenda kesi isijibu swali la nani aliyefyatua risasi
Waendesha mashtaka hawadai kwamba Davis ndiye aliyefyatua risasi usiku huo. Kwa hiyo, huenda kesi hiyo isithibitishe moja kwa moja ni nani aliyefyatua risasi zilizompiga Shakur.
Badala yake, waendesha mashtaka wanapanga kuthibitisha kwamba Davis alifanya mawasiliano na mipango iliyopelekea kuawa kwa Tupac Shakur, na kwamba ndiye aliyetoa silaha iliyotumika kumpiga risasi.
Waendesha mashtaka wanatarajia kuwaita mashahidi kati ya 35 na 45 wakati wa kesi hiyo. Mashahidi hao wanatarajiwa kujumuisha watu waliomuona Tupac Shakur muda mfupi kabla ya kupigwa risasi, pamoja na watu waliokuwa karibu na Tupac Shakur au Davis wakati wa tukio hilo.

















