Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya inawaonya viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kwamba itatekeleza kikamilifu Sheria ya Utulivu wa Umma huku nchi ikiingia katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, polisi walisema wamebaini visa vya kutovumiliana kisiasa, vurugu na uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.
NPS inasema kuwa yeyote anayepanga mkutano wa hadhara au maandamano lazima amjulishe mkuu wa polisi anayesimamia eneo husika angalau siku tatu na si zaidi ya siku 14 kabla ya tukio hilo.
Taarifa hiyo ya kutoa notisi lazima ijumuishe maelezo ya mratibu, ukumbi au njia ya maandamano, tarehe na muda. Mikutano ya hadhara na maandamano pia sharti yafanyike kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili jioni.
Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Polisi ya Kitaifa Muchiri Nyaga, ilisema taratibu hizi zinaiwezesha polisi kupanga vyema ulinzi na kuzuia makundi pinzani ya kisiasa kufanya matukio yanayokinzana katika eneo moja.
Hakuna aliye juu ya sheria
“Ni muhimu kutambua kuwa kutoa taarifa na kupata uthibitisho wa baadaye kuhusu mikutano yote inayokusudiwa kufanywa na wadau wa pande zote za kisiasa kwa afisa aliyeidhinishwa, ni hatua sahihi na halali inayoiwezesha polisi kutoa ulinzi madhubuti na wenye kuzingatia taarifa sahihi.”
Onyo hilo linakuja huku shughuli za kisiasa zikishika kasi kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2027, huku polisi wakisema kuwa vurugu, uchochezi na kuvuruga mikusanyiko halali havitavumiliwa.
Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) inaonya waziwazi kwamba watu wanaohusika na vurugu, kufadhili magenge ya uhalifu, kuchochea wafuasi au kuvuruga mikusanyiko halali “watashughulikiwa kwa ukali na kwa mujibu wa sheria.”
Inasema msimamo wake unahusu pande zote za kisiasa na kusisitiza kuwa jeshi la polisi litaendelea kutojihusisha na siasa na kutopendelea upande wowote.
“NPS inasisitiza tena kwa dhati kwamba hakuna mtu, bila kujali hadhi ya kijamii, mrengo wa kisiasa, au wadhifa wa umma, aliye juu ya sheria,” taarifa hiyo iliongeza.
Huduma hiyo inasema utendaji wake wa kazi utaongozwa na kuheshimu haki za binadamu, utu na uwajibikaji.
Taarifa hiyo inatoa onyo kwa wanasiasa wa Kenya huku kampeni zikishika kasi, na pia inaashiria kuwa polisi wanakusudia kutumia mbinu iliyopangwa zaidi katika kushughulikia mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya umma kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

















