Ajali ya basi katika Rasi ya Sinai mashariki mwa Misri imesababisha vifo vya watu 16 na kuwajeruhi wengine 28 siku ya Jumatano, wizara ya afya ilisema.
Ambulensi ishirini zilifika kwenye eneo hilo la ajali, lililoko kati ya miji ya kitalii ya Dahab na Nuweiba mashariki mwa pwani ya Sinai Kusini, wizara hiyo ilisema.
Miongoni mwa waliofariki ni raia 10 wa Jordan, kulingana na televisheni ya taifa ya nchini Jordan.
“Raia kumi wa Jordan wamefariki baada ya basi la abiria kupinduka katika barabara ya Dahab na Nuweiba kanda ya Misri ya Sinai Kusini ,” Shirika rasmi la habari la Jordan la Al-Mamlaka lilisema, likiongeza kuwa basi hilo lilikuwa limebeba jumla ya abiria 43, kati yao 22 walikuwa raia wa Jordan.
Mamlaka zinasema kuwa waliojeruhiwa walikuwa wanatibiwa, lakini hawakusema kuhusu chanzo cha ajali.
Eneo hilo ni maarufu kwa utalii kutokana na mandhari yake ya kupendeza.
Mwezi uliopita, watu wasiopungua 18, wengi wao wakiwa vijana, walifariki kaskazini mwa Misri wakati magari mawili yaliyokuwa na wafanyakazi wa shambani kugongana.
Mwaka uliopita, karibu watu 6,000 walifariki katika ajali mbali mbali za barabarani kote nchini, kulingana na shirika la takwimu la Misri.

















