Marekani inarejesha kiasi cha dola milioni 2.5 nchini Gambia kutokana na mauzo ya jumba la kifahari lililonunuliwa kwa fedha haramu na kiongozi wa zamani Yahya Jammeh pamoja na mkewe, Wizara ya Sheria ilisema Ijumaa.
Fedha hizo zitatumika “kuwalipa fidia waathiriwa wa utawala wa Jammeh,” wizara hiyo ilisema katika taarifa.
Jumba hilo, lililoko katika eneo la kifahari la Potomac, Maryland karibu na Washington, lilinunuliwa kwa kutumia “mapato ya uhalifu na fedha za umma za Gambia zilizofujwa,” ilisema taarifa hiyo.
“Kesi hii ni mfano muhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuwawajibisha wale wanaotumia mfumo wetu wa kifedha kujaribu kuficha mapato haramu yatokanayo na uhalifu,” alisema Naibu Mwanasheria Mkuu Tysen Duva.
Kushindwa katika uchaguzi
Miongo miwili ya utawala wa Jammeh, kuanzia mwaka 1994 hadi 2017, iligubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya mahitaji binafsi ya kiongozi huyo, kulingana na serikali ya sasa na makundi ya kutetea haki.
Kwa sasa Jammeh anaishi nchini Equatorial Guinea, baada ya kulazimishwa kuondoka madarakani kutokana na shinikizo kutoka kwa nchi jirani kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi wa mwaka 2016 dhidi ya Adama Barrow.
Jammeh, mkewe Zineb na watoto wao wamepigwa marufuku kusafiri kwenda Marekani tangu mwaka 2018.

















