Polisi nchini Afrika Kusini siku ya Jumamosi walipata mwili mwingine huko Ekurhuleni, mashariki mwa Johannesburg, na kufanya idadi ya wanawake waliopatikana wakiwa wamefariki katika eneo hilo kufikia kumi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Mwili huo ulipatikana katika eneo la makazi la Tembisa, polisi walisema, bila kutoa maelezo zaidi.
“Kwa sasa, tunaweza tu kuthibitisha kupatikana kwa mwili huo. Wataalamu wa kushughulikia eneo la tukio na wadau wote husika tayari wapo eneo la tukio,” alisema msemaji wa polisi, Brigedia Brenda Muridili.
Kituo cha televisheni cha eneo hilo, eNCA, kiliripoti kuwa mwili huo ulipatikana katika eneo la makaburi.
Washukiwa mikononi mwa polisi
Waathiriwa wengine tisa walikuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40, huku baadhi yao wakionyesha dalili za kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.
Mhanga wa kwanza, mwanamke mwenye umri wa miaka 37, alipatikana akiwa amefungwa kwa kamba za mnamo Julai 15. Mshukiwa mmoja alikamatwa siku mbili baadaye.
Washukiwa wengine wawili, wanawake wenye umri wa miaka 31 na 38, walikamatwa kuhusiana na kisa cha mhanga wa tisa na kufunguliwa mashtaka siku ya Jumatatu.
Polisi wamesema kuwa kisa hicho kinaweza kuwa kilitokana na suala la uhusiano.
Ukatili wa kijinsia ni tatizo sugu nchini Afrika Kusini, huku serikali ikiahidi kukabiliana na tatizo hilo na kulitangaza kuwa janga la kitaifa.

















