Afrika

Rais Museveni wa Uganda aanza rasmi muhula mpya

Rais Yoweri Museveni ambae ameingia madarakani mwaka 1986, huu utakuwa ni muhula wake wa saba kuliongoza taifa hilo.

Newstimehub

Newstimehub

12 Mei, 2026

b763662bcc04c81d8ceb8272cca63345ac7a658c6fb3292e3457b79856e492f8

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekula kiapo rasmi hii leo cha kuiongoza nchi hiyo katika muhula wake wa saba. Sherehe za kuapishwa zimefanyika katika viwanja vya Kololo jijini Kampala, na kushuhudiwa na wageni mbalimbali ikiwemo viongozi wa serikali na nchi.

Miongoni mwa viongozi kutoka eneo la Afrika Mashariki waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, na Felix Tshisekedi wa DRC. Rais wa Kenya aliwakilishwa na Naibu wa Rais Kithure Kindiki.

Viongozi wengine ni Rais wa Ethiopia Taye-Atske Selassie, pamoja na wakuu wa taasisi za kikanda. Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta pia alikuwepo kwenye hafla hiyo.

“Mimi Yoweri Kaguta Museveni, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa mwaminifu, na kwamba nitailinda na kudumisha katiba ya nchi,” aliapa Rais Museveni huku sauti za vifijo zikisikika kutoka kwa wananchi.

Rais Museveni ambae ameingia madarakani mwaka 1986, huu utakuwa ni muhula wake wa saba kuliongoza taifa hilo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, Rais Museveni alitangazwa mshindi kwa asilimia 71, na kuwashinda wagombea wengine akiwemo mpinzani wake Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kutoka Chama cha National Unity Platform ambae kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, aliambulia asilimia 24.7 ya kura.

Licha ya ushindi mkubwa alioupata Rais Museveni, alilalamika kuibiwa kura kwa madai kwamba, angeweza kupata ushindi mkubwa zaidi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu wamedai Uchaguzi huo, haukuwa wa haki na huru. Kwa upande wake, Bobi Wine, ambae punde tu baada ya Uchaguzi aliondoka nchini huko kwa madai ya kuhofia usalama wake, ameituhumu serikali ya Museveni kwa kukandamiza demokrasia.