Afrika

Ushelisheli kumchagua rais katika duru ya pili ya uchaguzi

Hakuna mgombea aliyepata asilimia 50 ya kura kuwezesha kupatikana kwa mshindi katika duru ya kwanza .

Newstimehub

Newstimehub

29 Septemba, 2025

97226e824309a39396d97cf4d361611ef47061a7ef0b5cbce719789baaf5dc95

Uchaguzi wa urais nchini Ushelisheli utaingia duru ya pili kati ya kiongozi wa upinzani Patrick Herminie na Rais aliyeko madarakani Wavel Ramkalawan baada ya kutopatikana mshindi katika duru ya kwanza, tume ya uchaguzi imesema.

Kiongozi wa chama cha upinzani, United Seychelles (US), Patrick Herminie, alipata asilimia 48.8 ya kura, huku Ramkalawan,wa chama cha Linyon Demokratik Seselwa (LDS), akiwa na asilimia 46.4%, tume ya uchaguzi ilitangaza siku ya Jumapili.

Ramkalawan amekuwa akitaka kupata ushindi ili azuie chama ambacho kimekuwa katika siasa za Ushelisheli kwa miongo minne kurudi tena madarakani.

Asilimia 50 ya kura

Hakuna mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika kwa ushindi wa duru ya kwanza.

Chama cha US pia kimepata viti zaidi katika bunge, vikishinda maeneo bunge 15 na viti vingine vinne zaidi kupitia uwakilishi wa mizania, na kuwapa wingi wa viti bungeni.

LDS imepata viti 11 vya maeneo bunge na viti vingine vinne vya uwakilishi, na kufanya chama tawala kuwa chama pinzani bungeni.

Katika uchaguzi wa urais, wagombea wawili wakuu sasa watakabiliana kwenye duru ya pili inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11 Oktoba. Mshindi atapata kuongoza kwa muhula wa miaka mitano.

Karibu asilimia 82 ya wapiga kura waliojisajili walishiriki kwenye duru ya kwanza, ambayo ilifanyika kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi, tume ya uchaguzi ilisema.