Serikali ya Somalia imetangaza mipango ya kuimarisha usalama katika mji mkuu, Mogadishu, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo. Uchaguzi huo unatajwa kuwa wa kihistoria, kwani ni mara ya kwanza kwa wananchi kupiga kura moja kwa moja katika ngazi ya mitaa baada ya takriban miaka 60.
Waziri wa Usalama wa Somalia, Abdullahi Sheikh Ismail, alisema zaidi ya maafisa 10,000 wa usalama watapelekwa Mogadishu ili kuhakikisha hali ya amani kabla na wakati wa zoezi la upigaji kura. Kwa mujibu wa serikali, hatua hiyo inalenga kulinda wapiga kura na kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila vurugu.
Mapema mwaka huu, Somalia ilianza kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa zoezi la usajili wa wapigaji kura, hatua inayolenga kuondoa mfumo wa awali wa uchaguzi wa njia isiyo ya moja kwa moja uliotegemea makabila. Mfumo huo ulikuwa ukitumika tangu kupinduliwa kwa serikali ya kijeshi ya Siad Barre mwaka 1969.
Uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika Desemba 25, utahusisha zaidi ya wagombea 1,600 wanaowania viti 390 vya serikali za mitaa katika mkoa wa Banadir. Hata hivyo, baadhi ya vyama vya upinzani vimetangaza kususia zoezi hilo, wakidai maamuzi muhimu yalifanywa na serikali bila mashauriano ya pamoja.
Tume ya Uchaguzi ya Somalia imesema takriban watu 400,000 tayari wamejisajili kupiga kura. Mwenyekiti wa tume hiyo, Abdikarin Ahmed Hassan, alisema kutakuwa na udhibiti mkali wa harakati siku ya uchaguzi, huku wapiga kura wakisafirishwa kwa mabasi hadi vituo vya kupigia kura.
Serikali imeeleza kuwa uchaguzi huo ni hatua muhimu kuelekea mfumo wa “mtu mmoja, kura moja”, ambao umecheleweshwa mara kadhaa mwaka huu. Somalia pia inatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais mwaka 2026, utakaohitimisha muhula wa Rais Hassan Sheikh Mohamud.
CHANZO: TRT Afrika














