Mamlaka za Uturuki zimetangaza kuwa kisanduku cheusi pamoja na kifaa cha kurekodi sauti za rubani vimepatikana kutoka kwenye mabaki ya ndege binafsi iliyoanguka karibu na mji wa Ankara usiku wa Jumanne, ajali iliyosababisha kifo cha Mkuu wa Jeshi wa Libya na watu wengine waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Akizungumza Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya, alisema kuwa vifaa hivyo muhimu vilipatikana kufuatia shughuli za uokoaji na uchunguzi zilizofanywa na maafisa wa Kituo cha Uchunguzi wa Usalama wa Usafiri chini ya Wizara ya Uchukuzi na Miundombinu.
Kwa mujibu wa Yerlikaya, kinasa sauti cha rubani kilipatikana majira ya saa 8:45 usiku, huku kisanduku cheusi kikigunduliwa dakika kadhaa baadaye saa 9:20 usiku katika eneo la ajali.
Aliongeza kuwa taratibu za kuchambua na kutathmini taarifa zilizomo kwenye vifaa hivyo tayari zimeanza ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Waziri huyo alisema jumla ya watu 408 walishiriki katika operesheni ya uokoaji na uchunguzi, wakitumia magari 103 pamoja na ndege saba.
Aidha, ujumbe wa watu 22 kutoka Libya, wakiwemo wanafamilia wa marehemu, wawakilishi wa Wizara ya Ulinzi na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani, tayari wamewasili mjini Ankara.
Yerlikaya alisema kuwa mamlaka za Uturuki pia zina nia kubwa ya kujua kilichosababisha ajali hiyo, akisisitiza kuwa taarifa kutoka kwenye kisanduku cheusi zitatoa mwanga juu ya chanzo cha tukio na matokeo yatatangazwa rasmi kwa umma.
Aliwasilisha pia salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha pamoja na serikali na wananchi wa Libya, akieleza tukio hilo kama ajali ya kusikitisha.
Awali, Yerlikaya alithibitisha kuwa mabaki ya ndege binafsi aina ya Falcon 50, iliyokuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Esenboga mjini Ankara kuelekea Tripoli, yalipatikana takribani kilomita mbili kusini mwa kijiji cha Kesikkavak, katika wilaya ya Haymana.
Kufuatia vifo hivyo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
CHANZO: TRT Afrika














