Papa Leo wa 14 ameongoza ibada ya mkesha wa Krismasi kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, katika hafla iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican, jijini Roma.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa kanisa akiwemo makardinali na maaskofu, pamoja na mabalozi, mapadre na waumini kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Katika hotuba yake ya homilia, Baba Mtakatifu alitumia nafasi hiyo kukosoa vikali tabia ya ubatili, akisisitiza kuwa si jambo la kibinadamu kuwatendea watu kana kwamba ni bidhaa au vitu vya kununuliwa na kuuzwa.
Kabla ya kuanza kwa ibada, Papa Leo XIV aliwasalimia waamini waliokuwa wamefurika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, akiwatakia heri ya Sikukuu ya Noeli na kuwataka kudumisha amani na mshikamano.
Tofauti na mtangulizi wake, Papa Leo alianza ibada ya mkesha huo muda mfupi kabla ya saa sita usiku na kuiongoza kwa muda mrefu zaidi, hatua ambayo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kidini wameitafsiri kama kurejea kwa baadhi ya mila za zamani za Kanisa Katoliki.
Katika maadhimisho ya Krismasi yenyewe siku ya Alhamisi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa ujumbe wake wa jadi wa “Urbi et Orbi”, unaolenga kutoa baraka na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu.
Papa Leo XIV, ambaye jina lake halisi ni Robert Francis Prevost, alichaguliwa kuwa Papa wa 267 wa Kanisa Katoliki tarehe 8 Mei 2025, akichukua nafasi hiyo baada ya kifo cha Papa Francis kilichotokea Aprili 21, 2025.
CHANZO: TRT Afrika














