Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ameituhumu Israel kwa kuitambua eneo lililojitenga la Somaliland kwa malengo ya kijeshi na mpango wa kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu, akisema hatua hiyo haina uhusiano wowote na amani ya kikanda.
Akizungumza katika mahojiano na Al Jazeera, Rais Mohamud alisema taarifa za kijasusi zinaonyesha kuwa Somaliland imekubali kuwapokea Wapalestina na kuruhusu kuanzishwa kwa kambi ya kijeshi ya Israel, kwa matarajio ya kutambuliwa kama taifa huru. Alieleza kuwa hatua ya Israel ilikuwa ya ghafla na ya kushangaza, ikiifanya kuwa nchi ya kwanza kuitambua Somaliland tangu ijitangaze kujitenga mwaka 1991.
Somalia imesisitiza kuwa Somaliland ni sehemu ya eneo lake la kikatiba, na imeonya kuwa mawasiliano ya moja kwa moja na eneo hilo ni ukiukaji wa mamlaka ya taifa. Rais Mohamud alisema serikali ya Mogadishu inaendelea kusukuma juhudi za kuunganisha nchi kwa njia ya amani.
Kwa mujibu wa rais huyo, Israel inalenga kudhibiti njia muhimu za majini katika Bahari ya Shamu, Ghuba na Ghuba ya Aden, huku utambuzi wa Somaliland ukitumiwa kuhalalisha uwepo wake wa siri katika eneo hilo. Aliongeza kuwa upinzani wa kimataifa unaongezeka, huku mataifa mengi yakilaani hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na tishio kwa uthabiti wa kikanda.
CHANZO: TRT Afrika














