Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, International Criminal Court, imeamuru kulipwa fidia ya takriban dola milioni 8.5 kwa waathirika wa uhalifu uliotekelezwa na kiongozi wa zamani wa wanamgambo nchini Mali.
Uamuzi huo unahusiana na kesi ya Al Hassan Ag Abdoul Aziz ambaye alipatikana na hatia mwaka 2024 kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mateso, unyanyasaji na ukandamizaji wa kidini.
Mahakama ilieleza kuwa zaidi ya watu 65,000 waliathiriwa na vitendo hivyo wakati wanamgambo walipodhibiti mji wa Timbuktu mwaka 2012.
Fidia hiyo itatolewa kwa mfumo wa pamoja, ikijumuisha msaada wa kijamii, elimu, mafunzo na huduma za afya ya akili kwa waathirika, hasa wanawake na wasichana ambao walipata madhara makubwa zaidi.
Ingawa mahakama imemtaja Al Hassan kuwa anawajibika kifedha, imethibitishwa kuwa hana uwezo wa kulipa, hivyo fedha hizo zitatolewa kupitia mfuko maalum wa kusaidia waathirika wa ICC.
Hatua hiyo inaonekana kama muhimu katika juhudi za kimataifa za kuhakikisha haki kwa waathirika wa migogoro na uhalifu mkubwa.
Chanzo:Africanews














