Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi atakutana na Rais wa Marekani Donald Trump pembeni mwa Kongamano la Uchumi Duniani mjini Davos, mkutano ambao utakuwa wa kwanza tangu Marekani itangaze mpango wake wa kumaliza vita vya Gaza.
Viongozi hao wawili walikutana mara ya mwisho Oktoba mjini Sharm el-Sheikh, wakati Misri iliandaa mkutano wa kusaini makubaliano ya kusitisha vita. Trump pia ametangaza kuwa yuko tayari kuanzisha tena upatanishi wa Marekani kati ya Misri na Ethiopia kuhusu mzozo wa Bwawa la Renaissance, ambalo Misri na Sudan wanaliona kama tishio kwa mgao wao wa maji ya Nile.
Mazungumzo ya awali yaliyoanzishwa na Marekani yalivunjika mwaka 2020 baada ya Ethiopia kujiondoa, ingawa baadaye yalihamishiwa chini ya Umoja wa Afrika. Bwawa hilo, lililozinduliwa rasmi mwaka jana, linatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 na kuongeza maradufu uwezo wa Ethiopia wa kuzalisha umeme. Ethiopia inaliona kama nyenzo ya kukuza uchumi wake, lakini Misri imepinga ikisema litapunguza mgao wake wa maji ya Nile, tegemeo kuu kwa kilimo na mahitaji ya zaidi ya watu milioni 100.
CHANZO: TRT Afrika














