Mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua za radi na theluji kali yamesababisha vifo vya angalau watu watano nchini Tunisia na Algeria.
Tunisia imeripoti vifo vya watu wanne mjini Moknine, kusini mwa mji mkuu Tunis, huku mvua kubwa ikilemaza usafiri, kusababisha kufungwa kwa shule katika mikoa 11 na kufungwa kwa balozi kadhaa. Taasisi ya hali ya hewa imetaja kiwango cha mvua kilichovunja rekodi, ikiwemo milimita 230 Monastir na 212 Zaghouan.
Nchini Algeria, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 60 alipoteza maisha kutokana na mafuriko ya ghafla katika wilaya ya Relizane. Mamlaka za ulinzi wa raia ziliokoa wakaazi waliokwama na kuonya kuwa mvua na upepo mkali utaendelea, pamoja na theluji katika maeneo ya milima.
Hali hii imekuja baada ya miaka ya ukame, na ingawa mabwawa yamejaa zaidi, mamlaka zinasema haitaweza kutatua upungufu wa maji wa muda mrefu.
CHANZO: TRT Afrika














