Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuasili mtoto mchanga wa kike aliyetelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora. Hafla ya kukabidhi mtoto huyo ilifanyika Machi 11, 2026 katika makazi ya rais yaliyopo Ikulu Chamwino.
Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu alikabidhiwa kwa rais na Mkuu wa Wilaya ya Nzega Naitapwaki Tukai.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mtoto huyo aliokotwa Januari 17, 2026 karibu na nyumba ya wageni ya Kasulu mjini Nzega baada ya kutelekezwa. Baadaye alipelekwa hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi huku jitihada za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio.
Rais Samia amesema atamhudumia mtoto huyo kwa kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama.
CHANZO: TRT Afrika














