Idara ya Upelelezi ya Marekani (FBI) imetangaza zawadi ya dola 200,000 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa afisa wa zamani wa Jeshi la Anga la Marekani, Monica Witt, ambaye anashutumiwa kuisaliti Marekani na kujiunga na Iran mwaka 2013.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, FBI imesema inaamini kuwa Witt bado anaendelea kushirikiana na shughuli za kijasusi za Iran hadi sasa.
“FBI haijamsahau, na tunaamini kuwa katika kipindi hiki muhimu cha historia ya Iran, kuna mtu anayejua alipo,” alisema Daniel Wierzbicki, mkuu wa kitengo cha kupambana na ujasusi wa FBI mjini Washington.
“Tunahitaji msaada wa wananchi ili kumkamata Witt na kumfikisha mbele ya mahakama,” aliongeza.
Monica Witt aliwahi kufanya kazi kama afisa wa kupambana na ujasusi katika Ofisi ya Uchunguzi Maalum ya Jeshi la Anga la Marekani. Kati ya mwaka 2003 na 2008 alihudumu katika operesheni mbalimbali za kijeshi na kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mwaka 2019, aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, John Demers, alisema kuwa Iran ilimshawishi Witt kujiunga nayo, kabla ya yeye kuikimbia Marekani na kuhamia upande wa Iran.
Maafisa wa Marekani walidai kuwa baada ya kujiunga na Iran, Witt alitoa taarifa nyeti za kiusalama, ikiwemo kufichua mpango wa siri wa ukusanyaji wa taarifa za kijasusi wa Marekani pamoja na kumtaja afisa mmoja wa ujasusi wa Marekani, jambo lililoweka maisha yake hatarini.
Waendesha mashtaka walieleza kuwa kati ya Januari 2012 na Mei 2015, Witt alishirikiana na maafisa wa Iran ndani na nje ya nchi hiyo kutoa nyaraka na taarifa zinazohusiana na usalama wa taifa la Marekani, huku akijua kuwa taarifa hizo zingeweza kutumiwa dhidi ya Marekani na kuisaidia Iran.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, baada ya kujiunga na Iran, Witt alipatiwa makazi, vifaa vya kompyuta na huduma nyingine na serikali ya Iran ili kusaidia shughuli zake.
Hadi sasa, haijulikani iwapo ana wakili wa kumtetea nchini Marekani.
















