Afrika

Misri yatoa wito kwa Marekani, Iran ‘kwa fursa’ ya makubaliano baada ya Trump kusitisha mashambulizi

Rais Donald Trump ametangaza “makubaliano muhimu” ya kumaliza vita Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Newstimehub

Newstimehub

12 Juni, 2026

c6832b29350a5eb49b3b6f01961cb292b2003bfb60b9a474ea1c1b5be42f21bf

Misri imetoa wito kwa Marekani na Iran kutumia kile walichokitaja kuwa “kutumia fursa iliopo” ya makubaliano ya kumaliza vita, baada ya Rais Donald Trump kusitisha vitisho vya mashambulizi zaidi kwa Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri alisema katika taarifa siku ya Alhamisi kuwa wanatarajia “fursa iliopo itatumiwa kufikia makubaliano ya masuala kadhaa na kuandaa mazingira ya kumaliza vita na kuanza hatua nyingine ya usalama katika kanda”.

Rais Donald Trump alitangaza kuhusu “makubaliano muhimu” ya kumaliza vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akisema anatarajia makubaliano hayo yatatiwa saini barani Ulaya pengine hata mwishoni mwa wiki hii.

Trump alisema Alhamisi kuwa Makamu wa Rais JD Vance atawakilisha Marekani.

Kusitisha mashambulizi

Maelezo ya kiongozi huyo wa Marekani yanakuja saa chache baada ya kuahidi kufanya mashambulizi mengine dhidi ya Iran, kabla ya kusitisha. Hakukuwa na thibitisho la hilo kutoka kwa Iran, na Trump hakutoa maelezo zaidi kuhusu ambacho kila upande kimekubaliana.

“Tumefikia makubaliano muhimu kuhusu vita na Iran,” Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.

Lakini msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei alisema Iran bado haijafanya maamuzi ya mwisho kuhusu uwezekano wa makubaliano na Marekani na haitokubali “masuala tata” katika majadiliano.

Baghaei anasema taarifa kuhusu wakati na sehemu ya kutia saini makubaliano bado haijaafikiwa na kwamba hakuna kilichothibitishwa.

Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya masuala ya makubaliano imekamilika lakini Marekani imekuwa ikibadilisha msimamo wake wakati wa mazungumzo.