Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, amesema hakuna suluhu ya kudumu nchini Sudan bila kuondolewa kwa wanamgambo wa RSF. Akizungumza mjini Port Sudan, Burhan alisisitiza kuwa mapendekezo yoyote yanayohusisha RSF ni njia ya kuahirisha mgogoro, akieleza kuwa suluhu pekee ni kundi hilo kujisalimisha au kuweka silaha chini.
Burhan aliongeza kuwa vita vimesababisha vifo vingi, uharibifu mkubwa na raia wote wa Sudan wameathiriwa. Alidai kuwa wito wa kusitisha mapigano uliongezeka baada ya kuanguka kwa mji wa Al Fasher Oktoba, akisema juhudi hizo zilitaka kuruhusu RSF kupanua udhibiti wake.
Sudan ilipendekeza Uturuki au Qatar kuwa wapatanishi, lakini RSF ilikataa. Burhan alisema pia nchi za kikanda kama Saudi Arabia na Misri zinaweza kushiriki katika juhudi za upatanishi, akisisitiza imani yake kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan.
Aidha, Burhan alisisitiza kuwa RSF na jeshi la Sudan si nguvu zilizo sawa, akitaja kundi hilo kuendelea kusafirisha silaha kwa njia za magendo na kufanya mashambulizi licha ya maazimio ya Umoja wa Mataifa. Alisema jeshi na wananchi wa Sudan wameazimia kuiondoa RSF na wako tayari kwa suluhu zote za amani.
CHANZO: TRT Afrika














