Jeshi la Israel limefanya mashambulizi ya anga siku ya Jumatano katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya Mashariki ya Kati ambayo pia yanajumuisha Lebanon.
Shirika la Habari la National News Agency nchini Lebanon limesema ndege za kivita za Israel zilishambulia eneo la Nabatieh al-Fawqa pamoja na viunga vya mashariki vya mji jirani wa Kfar Tebnit.
Kwa mujibu wa shirika hilo, Israel pia ilifanya shambulio la ndege isiyo na rubani katika mji wa Ansariyeh ulioko eneo la Zahrani.
Ingawa vurugu zimepungua nchini Lebanon tangu kutangazwa kwa makubaliano ya Marekani na Iran ya kusitisha vita vya Mashariki ya Kati siku ya Jumatatu, hata hivyo mashambulizi ya Israel kusini mwa nchi hiyo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua watano tangu makubaliano hayo yalipoanza kutekelezwa.
Kupungua kwa mapigano kumewawezesha baadhi ya wakazi wa kusini mwa Lebanon kurejea katika miji na vijiji vyao ili kukagua hali ilivyo. Hata hivyo, jeshi la Lebanon limewasihi wananchi kuchelewesha kurejea kwao kutokana na “hatari ya ukiukaji wa makubaliano na mashambulizi kutoka kwa Israel”.
Lebanon ilijuiunga katika vita vya Mashariki ya Kati mapema mwezi Machi baada ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran kurusha makombora kuelekea Israel, likisema ni kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel.
Israel ilijibu kwa kuanzisha kampeni kubwa ya mashambulizi ya anga pamoja na uvamizi wa ardhini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema Jumanne kuwa kumalizika kwa mzozo huo hakutakamilika “bila kuondolewa kwa majeshi ya Israel katika maeneo iliyoyakalia wakati wa vita hivi”.
“Kwa mtazamo wetu, shambulio lolote la kijeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon kuanzia sasa, pamoja na kuendelea kwa ukaliaji wa maeneo ya Lebanon, litachukuliwa kuwa ukiukaji wa makubaliano ya maelewano,” alisema.
Kiongozi wa kundi hilo, Naim Qassem, anatarajiwa kutoa hotuba kupitia televisheni siku ya Jumatano.
Siku ya Jumanne, Qassem alieleza “shukrani za dhati” kwa juhudi za Iran za “kuilazimisha Israel kusitisha mara moja operesheni zake za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon”.
Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza Jumanne kuwa idadi ya waliouawa katika mashambulizi ya Israel tangu kuzuka kwa vita imefikia watu 3,826, huku waokoaji wakiendelea kutoa miili zaidi kutoka chini ya vifusi.

















