Serikali ya Libya imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Mkuu wa Jeshi, Mohammed al-Haddad, pamoja na maafisa wengine wanne waandamizi wa kijeshi, waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea karibu na mji wa Ankara, nchini Uturuki.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilieleza masikitiko makubwa kwa msiba huo na kutoa pole kwa familia za waliopoteza maisha pamoja na wanajeshi wenzao katika Vikosi vya Ulinzi vya Libya.
Serikali ilisema kuwa katika kipindi cha maombolezo, bendera katika taasisi zote za umma zitapeperushwa nusu mlingoti, huku shughuli na hafla rasmi zikisimamishwa kwa muda huo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa serikali inaungana na familia za marehemu kwa majonzi, ikiomba rehema kwa waliopoteza maisha na subira kwa ndugu zao.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Urais la Libya, Mohamed Menfi, alithibitisha vifo vya Mohammed al-Haddad na maafisa wanne wa kijeshi waliokuwa naye katika ndege hiyo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Menfi alielezea tukio hilo kama pigo kubwa kwa taasisi ya kijeshi ya Libya na kwa taifa kwa ujumla, akiwataja marehemu kama viongozi waliolitumikia taifa kwa uaminifu, nidhamu na kujitolea katika nyakati nyeti.
Menfi pia alituma salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa na kwa wanachama wa vikosi vya ulinzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya, alisema kuwa mabaki ya ndege binafsi aina ya Falcon 50 iliyokuwa ikisafiri kuelekea Tripoli yalipatikana kusini mwa wilaya ya Haymana, karibu na Ankara.
CHANZO: TRT Afrika














