Marekani imeanza kuendesha kwa kasi safari za ndege za kukusanya taarifa za kijasusi katika maeneo mbalimbali ya Nigeria tangu mwishoni mwa Novemba, kulingana na taarifa za ufuatiliaji wa ndege na vyanzo vya sasa na vya zamani vya serikali ya Marekani. Hatua hiyo inaashiria kuimarika kwa ushirikiano wa kiusalama kati ya Washington na Abuja.
Ingawa Reuters haikuweza kubaini kwa uhakika aina ya taarifa zinazokusanywa, operesheni hiyo imeanza muda mfupi baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa kauli nzito akitishia uwezekano wa kuingilia kijeshi Nigeria, akidai nchi hiyo imeshindwa kuzuia mashambulizi dhidi ya Wakristo.
Takwimu zinaonyesha kuwa ndege hizo, zinazoendeshwa na wakandarasi wa Marekani, huondoka Ghana, huruka juu ya Nigeria na kisha kurejea Accra. Ndege hizo zinaendeshwa na kampuni ya Tenax Aerospace yenye makao yake Mississippi, inayojihusisha na misheni maalum na kushirikiana kwa karibu na jeshi la Marekani. Kampuni hiyo haikutoa maoni kuhusu suala hilo.
Mchambuzi wa masuala ya usalama wa Afrika katika Taasisi ya American Enterprise, Liam Karr, alisema operesheni hiyo inaendeshwa kutoka uwanja wa ndege wa Accra, unaotumika kama kitovu cha shughuli za kijeshi za Marekani barani Afrika. Aliongeza kuwa safari hizo zinaashiria juhudi za Marekani kurejesha uwezo wake wa ujasusi katika eneo hilo, kufuatia uamuzi wa Niger wa kuwataka wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo mwaka jana.
Afisa mmoja wa zamani wa Marekani alisema baadhi ya vifaa vya anga vilihamishiwa Ghana mwezi Novemba chini ya utawala wa Trump, ingawa idadi kamili ya ndege zinazotumika haijulikani. Afisa wa sasa wa Marekani alithibitisha kuwepo kwa safari hizo juu ya Nigeria lakini hakutoa maelezo zaidi kwa sababu za kidiplomasia.
Pentagon ilisema ilifanya mazungumzo yenye mafanikio na Nigeria baada ya kauli ya Trump, lakini ilikataa kutoa taarifa kuhusu shughuli za kijasusi. Jeshi la Nigeria na maafisa wa Ghana hawakujibu maombi ya maoni.
Chanzo cha usalama cha Nigeria kilieleza kuwa Marekani ilikubali kuweka vifaa vya anga kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa katika mkutano uliofanyika Novemba 20 kati ya Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Nigeria, Nuhu Ribadu, na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth.
Taarifa za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa ndege ya aina ya Gulfstream V, iliyorekebishwa kwa kazi za ujasusi, imekuwa ikiruka juu ya Nigeria karibu kila siku tangu kuanza kwa operesheni hiyo.
Hatua hii inakuja wakati Nigeria ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama. Rais Bola Tinubu alitangaza hali ya tahadhari mwezi uliopita na kuamuru kuajiriwa kwa maelfu ya wanajeshi na polisi kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya silaha, mauaji na visa vya utekaji nyara, ikiwemo kutekwa kwa zaidi ya wanafunzi 300 kaskazini mwa nchi.
Marekani na Nigeria pia zimeunda kikosi kazi cha pamoja cha kushughulikia masuala ya usalama, hatua inayolenga kukabiliana na hali tete ya ulinzi nchini humo.
CHANZO: TRT Afrika














