Wafanyabiashara wakubwa wa sekta ya mafuta wamekanusha vikali madai ya kutoa rushwa kwa aliyekuwa waziri wa mafuta wa Nigeria, Diezani Alison-Madueke.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama nchini Uingereza, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa ili kupata mikataba ya serikali katika sekta ya mafuta. Hata hivyo, wameeleza wazi kuwa hawakutoa fedha wala zawadi yoyote kwa waziri huyo.
Upande wa mashtaka unadai kuwa waziri huyo alipokea manufaa mbalimbali ikiwemo makazi ya kifahari, safari za ndege binafsi na matumizi makubwa ya fedha wakati alipokuwa madarakani kati ya mwaka 2010 na 2015.
Hata hivyo, Diezani Alison-Madueke naye amekanusha tuhuma hizo, akisema hakuwahi kutumia vibaya madaraka yake wala kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama ya Southwark Crown Court jijini London imevutia umakini mkubwa kimataifa, hasa kutokana na umuhimu wa sekta ya mafuta katika uchumi wa Nigeria.
Wachambuzi wanasema kuwa kesi hii inaweza kuwa na athari kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa katika sekta ya nishati barani Afrika, huku ikionyesha jinsi kesi za kifısadi zinavyoweza kufikishwa katika mahakama za kimataifa.
Chanzo:Africanews














