Mfalme wa Moroko, Mohammed VI, amemteua mwanawe, Moulay Hassan, kushika wadhifa wa juu katika sekta ya ulinzi wa taifa.
Uteuzi huo unatajwa kuwa na uzito mkubwa katika mfumo wa uongozi wa Morocco, hasa kutokana na nafasi ya familia ya kifalme katika kusimamia masuala ya kijeshi na usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa taarifa za kifalme, hatua hiyo inalenga kumpa mrithi huyo uzoefu wa moja kwa moja katika masuala ya ulinzi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya majukumu makubwa zaidi ya uongozi katika siku zijazo,Moulay Hassan, ambaye tayari amekuwa akionekana kushiriki katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa, sasa anatarajiwa kuwa na jukumu kubwa zaidi katika kusaidia kusimamia sera na mikakati ya kijeshi ya nchi hiyo.
Wachambuzi wa siasa wanasema uteuzi huo unaonyesha namna Morocco inavyoandaa kizazi kijacho cha uongozi kwa njia ya hatua kwa hatua, hasa katika sekta nyeti kama ulinzi na usalama.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa uteuzi kama huo unazingatia uwazi na utaalamu ili kuimarisha imani ya umma katika taasisi za serikali.
Hatua hiyo pia inaonekana kama ishara ya kuimarisha uthabiti wa taasisi za kifalme na kuhakikisha mwendelezo wa sera za kitaifa.
Chanzo:Africanews
















