Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia wanaendelea na mashauriano kuhusu rasimu ya makubaliano ya ulinzi, baada ya takribani mwaka mmoja wa mazungumzo ya kidiplomasia. Waziri wa Pakistan Raza Hayat Harraj amesema rasimu hiyo tayari ipo kwa pande zote tatu na imekuwa ikijadiliwa kwa miezi kadhaa, ikilenga kuimarisha ushirikiano wa kiusalama katika eneo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amethibitisha kuwa mazungumzo yamefanyika, lakini akasisitiza kuwa hakuna makubaliano yaliyotiwa saini hadi sasa. Fidan ameeleza kuwa mashauriano hayo yanapaswa kuangaliwa katika muktadha mpana wa ushirikiano wa kikanda, badala ya kuunda muungano mdogo wa kijeshi.
Harraj ameongeza kuwa makubaliano hayo yanadhihirisha maslahi ya pamoja ya mataifa hayo matatu katika kuimarisha usalama, hususan wakati huu ambapo eneo linakabiliwa na changamoto za kiusalama. Hivi karibuni, Saudi Arabia na Pakistan tayari wamesaini mkataba wa kimkakati wa ulinzi wa pamoja, wakiahidi kushirikiana iwapo taifa moja litashambuliwa.
Kauli kutoka Ankara na Islamabad zinaonyesha kuwa mawasiliano ya kidiplomasia yanaendelea, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa kujenga imani na kuunda jukwaa la ushirikiano wa muda mrefu.
CHANZO: TRT Afrika














