Kiongozi wa vikundi vya silaha mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, ameonesha masikitiko makubwa kufuatia kifo cha Mkuu wa Jeshi la Libya, Mohammed al-Haddad, aliyefariki pamoja na maafisa wengine wanne waandamizi wa kijeshi katika ajali ya ndege iliyotokea karibu na mji wa Ankara, nchini Uturuki.
Kupitia ujumbe alioutoa Jumanne, Haftar alieleza huzuni yake kubwa kutokana na msiba huo na kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya jenerali huyo pamoja na wananchi wote wa Libya.
Kwa upande wake, Bunge la Wawakilishi lenye makao yake Benghazi nalo lilitoa taarifa ya kuomboleza vifo vya Haddad na ujumbe wake, likieleza pole kwa familia zao na kwa jeshi la Libya kwa ujumla.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuenzi maisha ya marehemu na maafisa waliokuwa pamoja naye.
Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya, alithibitisha kuwa mabaki ya ndege binafsi aina ya Falcon 50, iliyokuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Esenboga mjini Ankara kuelekea Tripoli, yalipatikana na vyombo vya usalama takribani kilomita mbili kusini mwa kijiji cha Kesikkavak, wilayani Haymana.
CHANZO: TRT Afrika














