Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah, kufuatia ajali mbaya ya ndege iliyotokea jijini Ankara na kusababisha kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Libya, Jenerali Mohammed Ali Al-Haddad.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, Rais Erdogan alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu Dbeibah siku ya Jumatano, ambapo alieleza masikitiko na huzuni yake kubwa juu ya kupoteza maisha ya Jenerali Al-Haddad pamoja na waliokuwa wakisafiri naye.
Duran alisema kuwa Erdogan alisisitiza mshikamano wa Uturuki na Libya katika kipindi hiki kigumu, huku akitoa pole kwa serikali na wananchi wa Libya kufuatia msiba huo.
Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya, alithibitisha kuwa mabaki ya ndege hiyo aina ya Falcon 50, iliyokuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Esenboga jijini Ankara kuelekea Tripoli, yaligunduliwa karibu kilomita mbili kusini mwa eneo la Kesikkavak katika wilaya ya Haymana, Ankara.
Yerlikaya pia alisema kuwa kisanduku cheusi cha ndege pamoja na kifaa cha kurekodi sauti vilipatikana siku ya Jumatano, na uchunguzi wa kitaalamu tayari umeanza ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya marehemu na waathirika wengine wa ajali hiyo.
CHANZO: TRT Afrika














