Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o, amesimamishwa kushiriki mechi nne na kutozwa faini ya dola 20,000 na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Hatua hiyo imechukuliwa baada ya tukio la utovu wa nidhamu wakati wa mechi ya Cameroon dhidi ya Morocco iliyomalizika kwa mabao 2-0 katika mashindano ya AFCON.
Eto’o anaripotiwa kuonyesha ishara ya hasira kutokana na maamuzi ya waamuzi mbele ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe. Tukio hilo lilitokea sambamba na mvutano kati ya wachezaji wa pande zote mbili, jambo lililosababisha CAF kufungua uchunguzi kuhusu vurugu zilizojitokeza katika baadhi ya mechi za AFCON.
FECAFOOT imepinga uamuzi huo, ikisema mchakato wa kinidhamu haukuwa wa haki na hauna maelezo ya wazi. Shirikisho hilo limeahidi kukata rufaa huku likisisitiza kuwa linaendelea kumuunga mkono rais wake.
CHANZO: TRT Afrika














