Shirika la Tunisian League for Human Rights (LTDH), mojawapo ya mashirika yaliyoshinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2015, limesimamishwa shughuli zake kwa muda wa mwezi mmoja nchini Tunisia.
Rais wa shirika hilo, Bassem Trifi, amesema amri ya kusimamishwa ilitolewa na mahakama ya mwanzo ya Tunis na kwamba shirika hilo litakata rufaa kupinga uamuzi huo.
LTDH imeeleza kuwa ilisimamishwa kwa madai ya kuwepo kwa kasoro za kiutawala, lakini imeutaja uamuzi huo kuwa wa hatari na wa kiholela.
Shirika hilo limesisitiza kuwa litaendelea kupigania haki na uhuru licha ya hatua hiyo.
LTDH ni sehemu ya kundi la Tunisian National Dialogue Quartet lililotunukiwa Tuzo ya Nobel kwa mchango wake katika mpito wa kidemokrasia wa Tunisia baada ya mapinduzi ya mwaka 2011.














