Afrika

Sierra Leone yakubali kupokea kundi la kwanza la wahamiaji wanaofukuzwa Marekani

Sierra Leone ni nchi ya hivi karibuni barani Afrika ambayo imeingia makubaliano kama hayo na Marekani, na itapokea ufadhili wa dola milioni 1.5 kusaidia mpango huo.

Newstimehub

Newstimehub

20 Mei, 2026

f087c1409c4e42c07cfcd8e38e9cadb9f8a7d2db5a7bacbd0c1e170ac204167f

Siku ya Jumatano, Sierra Leone itapokea kundi la kwanza la wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Marekani, wakati serikali ya Rais Donald Trump ikiendelea na mpango wa kuwarudisha wahamiaji kwenda katika nchi zinazoendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone, Timothy Musa Kabba, alisema kuwa ndege ya kwanza itabeba wahamiaji 25 na itawasili katika mji mkuu Freetown Jumatano asubuhi. Hii ni sehemu ya makubaliano ya nchi hiyo kupokea hadi wahamiaji 300 kwa mwaka wenye asili ya Afrika Magharibi.

Sierra Leone inakuwa miongoni mwa nchi nyingine za Afrika ambazo zimekuwa na makubaliano kama hayo na Marekani, zikiwemo Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eswatini, Equatorial Guinea, Ghana, Rwanda na Sudan Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje huyo, alisema: “Tunawapokea wahamiaji kwa sababu wanatoka Afrika Magharibi, na baadhi wana nyaraka za Sierra Leone walizokuwa nazo miaka mingi iliyopita.”

Kipindi cha siku 90

Wahamiaji hao wataruhusiwa kukaa nchini kwa muda wa siku 90, na baadaye wanaweza kusafiri kurudi katika nchi zao za asili.

Marekani itatoa dola milioni 1.5 kusaidia gharama za kibinadamu na za uendeshaji wa mpango huo.

Kwa kawaida, nchi za Afrika zinazokubali kupokea wahamiaji wasio na hati kutoka Marekani hupata ufadhili wa Marekani kama sehemu ya makubaliano hayo. Baadhi ya nchi, kama ya DRC, zimekubali pia kupokea wahamiaji kutoka maeneo mengine kama Amerika ya Kusini.