Serikali ya Sudan imeanza kupitia upya mikakati ya kujenga upya mji mkuu wa Khartoum na kurejesha huduma muhimu, baada ya kuamua kuhamishia tena shughuli zake katika mji huo uliokuwa umeathirika vibaya na mapigano.
Mjadala huo ulifanyika mjini Khartoum kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Mpito, Abdel Fattah al-Burhan, na Waziri Mkuu Kamel Idris, siku moja tu baada ya serikali kutangaza kurejea rasmi katika mji mkuu kwa mara ya kwanza tangu mapigano na vikosi vya RSF kuanza Aprili 2023.
Katika kipindi cha machafuko, serikali ilikuwa imehamishia shughuli zake Port Sudan, mji wa pwani ya Bahari Nyekundu, kufuatia uharibifu mkubwa na wakazi wengi kukimbia makazi yao.
Taarifa ya Baraza la Mpito imesisitiza kuwa mkutano huo ulilenga kuanzisha hatua za kufufua miundombinu na huduma za msingi, ili kurahisisha kurejea kwa wananchi katika makazi yao.
Burhan na Idris pia wamejadili mpango mpana wa kufungua tena taasisi za serikali kuu, wakisisitiza mshirikiano kati ya mamlaka na jamii ili kushinda changamoto na kuharakisha ujenzi wa mji.
Mazungumzo haya yamefuata tangazo la jeshi la Sudan la mwezi Mei, lililodai kurejesha udhibiti wa Khartoum na kufukuza vikosi vya RSF kutoka eneo hilo.
CHANZO: TRT Afrika














