Afrika

Watu 11 wakamatwa kufuatia mauaji ya risasi katika mgahawa Afrika Kusini

“Tume fanikiwa kuwakamata washukiwa 11 wanaohusishwa moja kwa moja na shambulio la risasi lililoua watu tisa Bekkersdal,” alisema Naibu Kamishna wa Polisi wa Mkoa, Meja Jenerali Fred Kekana.

Newstimehub

Newstimehub

25 Desemba, 2025

199

Polisi wa Afrika Kusini wamefanikiwa kuwakamata washukiwa 11 wanaohusishwa na tukio la ufyatuaji risasi lililoua watu tisa katika mgahawa mmoja eneo la Bekkersdal, karibu na mji wa Johannesburg, usiku wa Jumapili.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa moja usiku, wakati watu wasiojulikana wapatao 12 walivamia eneo hilo na kuanza kufyatua risasi ovyo, hali iliyozua taharuki kubwa kwa wakazi waliokuwepo.

Akizungumza Jumatano, Naibu Kamishna wa Polisi wa Mkoa, Meja Jenerali Fred Kekana, alisema kati ya waliokamatwa, tisa ni raia wa Lesotho, mmoja anatoka Msumbiji, huku mshukiwa mwingine akiwa raia wa Afrika Kusini anayedaiwa kufanya kazi migodini.

Ingawa awali shambulio hilo lilionekana kutokuwa na sababu ya wazi, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji hayo yalihusishwa na mivutano kuhusu uchimbaji haramu wa madini.

Wakati wa shambulio hilo, washambuliaji waliendelea kufyatua risasi huku watu wakikimbia kutafuta usalama. Mbali na waliokuwemo ndani ya mgahawa, dereva mmoja wa teksi pia aliuawa alipokuwa karibu akiwashusha abiria.

Baada ya operesheni ya kuwakamata washukiwa, polisi walipata silaha kadhaa zisizo halali, zikiwemo bunduki za kivita aina ya AK-47.

Afrika Kusini imeendelea kukumbwa na matukio ya mauaji ya risasi, ambayo mara nyingi husababishwa na uhalifu, vurugu za magenge na migogoro ya kiuchumi. Tukio hili linakuja wiki mbili tu baada ya shambulio jingine la risasi katika eneo la Saulsville, Pretoria, lililosababisha vifo vya watu 11 akiwemo mtoto wa miaka mitatu.

CHANZO: BBC NEWS