Wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, Morocco, wameanza mashindano hayo kwa kishindo baada ya kuifunga Comoro mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, jijini Rabat.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Morocco walivunja ukimya dakika ya 55 kupitia Brahim Diaz, aliyeipatia timu yake bao la kwanza. Ayoub El Kaabi alihakikisha ushindi kwa kufunga bao la pili dakika ya 74, matokeo yaliyowaweka Simba wa Atlas kileleni mwa Kundi A.
Ushindi huo umeipa Morocco mwanzo mzuri katika harakati za kulinyakua taji lao la AFCON wakiwa nyumbani. Kundi A pia linajumuisha timu za Zambia na Mali, ambazo zinatarajiwa kukutana Jumatatu.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, Comoro itakutana na Zambia Desemba 26, huku Morocco ikicheza dhidi ya Mali siku hiyo hiyo. Mechi za mwisho za kundi zitachezwa Desemba 29, ambapo Zambia itapambana na Morocco, na Comoro itakutana na Mali.
Mashindano ya AFCON 2025 yanashirikisha jumla ya timu 24 na yanafanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026. Timu mbili bora kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya 16 bora, pamoja na timu nne bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
CHANZO: TRT Afrika














