Huku Tanzania ikijitayarisha kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba29, 2025 kuna mambo kadhaa ambayo yanatofautisha uchaguzi uliopita.
Tangu kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi, na kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo huo mwaka 1995, nchi hiyo mpaka sasa imefanya jumla ya uchaguzi mara sita.
Chama cha Mapinduzi CCM ambacho ndicho kikongwe zaidi nchini humo kimekuwa kikishinda mara zote hivyo kukifanya kuwa moja ya vyama vinavyoendelea kutawala kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Licha ya chama hicho kuwa madarakani kwa muda wote, hii ndio mara ya kwanza kuwa na mgombea urais mwanamke, ambae ndie Rais wa sasa.
Rais Samia ambae awali alikuwa Makamu wa Rais, alishika nafasi hiyo baada ya kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli.
Hata hivyo, vyama vyengine vya kisiasa vimewahi kuweka wagombea urais wa kike.Wakati heka heka za kampeni zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi, tofauti na uchaguzi uliopita, uchaguzi wa mwaka huu, unafanyika bila uwakilishi wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA.
Hii ni baada ya CHADEMA kukataa kusaini Kanuni za Maadini ya Uchaguzi hivyo kujitoa rasmi katika ushiriki wa uchaguzi mkuu.
Lakini mbali na hivyo, uchaguzi wa mwaka huu pia, unafanyika huku mwenyekiti wa chadema Tundu Lissu akiwa kuzuizini kwa zaidi ya siku 100 ambapo ameshikiliwa kwa mashtaka kadhaa ikiwemo lile la uhaini.

Mashtaka ambayo Lissu ameyakana huku vute nikuvute ya kisheria ikiendelea.
Tofauti na uchaguzi uliopita, ambapo marais kadhaa wastaafu walikuwepo, Uchaguzi wa mwaka huu, utafanyika ukishuhudiwa na rais mmoja tu mstaafu, ambae ni Jakaya Mrisho Kikwete, hii ni baada ya waliotangulia kufarikia dunia katika nyakati tofauti.
Kwa upande wa Zanzibar, uchaguzi wa mwaka huu pia utakosa shamrashamra za aliyekuwa mwanasiasa mkongwe Maalim Seif Sharif Hamad, ambae nae alifariki dunia mwaka 2021.
Ni uchaguzi wa kwanza kuandaliwa na Tume inayodaiwa kufanyikwa madaliko, hivyo kuitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania INEC.
Kwa mara ya kwanza INEC, imetoa magari kwa wagombea wa nafasi ya urais ili kuweka mazingira ya usawa kwa wagombea wote.
Uchaguzi wa 2025 umewavutia wapiga kura zaidi, tofauti na ule uliopita wa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa INEC, kuna jumla ya wapiga kura 37,655,559 waliojisali, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na idadi ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.














