Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, yuko Florida kwa mazungumzo muhimu na Rais wa Marekani, Donald Trump, yanayolenga hali ya Ukanda wa Gaza na mpango wa nyuklia wa Iran. Netanyahu anatarajiwa pia kukutana kando na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.
Masuala ya usalama wa kikanda yanatawala ajenda ya mazungumzo hayo, yakihusisha mustakabali wa Gaza, hatima ya mpango wa makombora wa Iran, hali ya usalama nchini Lebanon na suala la kunyang’anywa silaha kwa kundi la Hezbollah.
Huu ni mkutano wa tano wa Netanyahu nchini Marekani tangu arejee madarakani. Unafanyika wakati Rais Trump akiweka msisitizo katika utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza unaotarajiwa kuanza mwezi ujao, huku Netanyahu akisisitiza zaidi kile anachokitaja kama tishio la Iran.
Awamu ya kwanza ya mpango wa Gaza, uliokubaliwa Oktoba, ilijumuisha usitishaji mapigano, kupunguzwa kwa uwepo wa jeshi la Israel Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu. Awamu inayofuata inalenga kuundwa kwa serikali ya kitaalamu Gaza, kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha usalama na mchakato wa kunyang’anywa silaha kwa Hamas.
Israel imesisitiza kuwa ujenzi upya wa Gaza hautaanza kabla ya Hamas kunyang’anywa silaha kikamilifu na suala la mateka kutatuliwa, huku baadhi ya hatua kama ufunguzi kamili wa mpaka wa Rafah zikiendelea kuwa na mvutano.
CHANZO: BBC NEWS














